Mtu yeyote anaweza kukimiliki. Ni kidogo na
rahisi kubebeka. Kimetengenezwa na kampuni maarufu ya huduma za mitandao ya
kompyuta ya Google ya nchini Marekani.
Kifaa hicho chaweza kuvaliwa kama miwani na
kimetengenezwa kwa teknolojia inayomwezesha mmiliki kusambaza sauti na picha
kwenye mitandao ya kompyuta kwa sekunde moja tu na kumfikia mtu yeyote akiwa
sehemu yoyote duniani.
Ni teknolojia ambayo imekusudiwa kuanza kutumika
duniani mwanzoni mwa mwaka ujao, hivyo kuleta changamoto nyingine ya
mawasiliano duniani.
Hii itasaidia watu kuweza kuwasiliana kirahisi na
wenzao kwa kutumia sauti na picha. Kinachofanyika ni kwamba mtu mwenye kifaa
hicho anaweza kuchukua sauti na picha za matukio kwenye eneo alipo.
Picha na sauti hizo ataweza kuziingiza kwenye
mtandao wa mawasiliano ya kompyuta kwenye wafuti au mitandao ya kijamii kama
vile blogu, facebook na twitter, hivyo kuwafanya watu wote wanaozitembelea
kuona picha na hata kusikia sauti.
Vifaa hivyo vimeambatanishwa kwenye fremu ambayo
mtumiaji atavaa kama miwani. Si lazima miwani hiyo iwe na kioo, hivyo kwa wale
wasiopenda kutumia miwani wanaweza kuitumia.
Kifaa hicho kinaweza kuambatanishwa na miwani ya
kawaida ama ile ya kuzuia mwanga mkali. Ndiyo maana kimepewa jina Google Glass
ama kwa tafsiri isiyo rasmi Miwani ya Google.
Kwa namna kinavyofanya kazi ni sawa na kompyuta
ama simu hasa kutokana na kuwa na kioo cha kuona. Kina kamera na kinasa sauti
na kina uwezo wa kujiunga na mawasiliano ya mtandao wa kompyuta kwa kutumia
programu ya Wife ambayo hauhitaji waya kuunganishwa.
Kifaa hicho kina kioo kidogo kilichowekwa juu ya
jicho moja, ambacho mtumiaji hukitumia kuangalia namna anavyojiunga kwenye
mtandao wa mawasiliano.
Kioo hicho ni sawa na kile cha simu au cha
kompyuta lakini ni kidogo sana ingawa kwa kuwa kipo karibu sana na jicho
humfanya mtumiaji kuona kwa ukubwa namna anavyoingia kwenye mtandao wa kompyuta
na kujiunga na eneo la mawasiliano alilokusudia.
Kifaa hicho kinatumia teknolojia ya kugusa ama
kama ilivyozoelaka ‘touch’. Mguso huo wa kupapasa haufanyiki kwenye kioo kama
ilivyo kwenye simu bali pembeni sambamba na eneo la fremu ya miwani
inayojishikilia juu ya sikio.
Kwa kupapasa, mtumiaji anaweza kutembelea wavuti
mbalimbali ama kutafuta sehemu yake ya mawasiliano kwa kutumia mtandao wa
Google.
Mtumiaji akiingia kwenye mtandao aliokusudia,
hapa anaweza kutumia teknolojia mpya ya Google kuunganisha mawasiliano na
kuanza kuingiza picha na sauti kama anavyopenda.
Teknolojia hiyo imefanyiwa majaribio kwenye
maeneo mbalimbali duniani na wengi wameikubali kwa kuwa itasaidia mawasiliano
ya papo kwa papo kama inavyojulikana kwa wengi, kupata matukio ‘live’.
Bei halisi ya kifaa hicho bado haijafahamika
ingawa tathmini za awali zinakikadiria kuuzwa kwa wastani wa Dola za Marekani
1,500 sawa na Sh2.4 milioni.
Hofu ya matumizi
Mitandao mbalimbali ya kompyuta iliyoripoti
mijadala mbalimbali sehemu ambazo Google Glass kimefanyiwa majaribio, wamekuwa
na wasiwasi kwamba kinaweza kutumika katika kuingilia uhuru binafsi wa mtu
pamoja na kusambaza picha za ngono.
Mmoja wa wataalamu wa kampuni ya Google aliwatoa
wasiwasi akisema wataweka programu maalumu ya kusimamia mawasiliano itakayozuia
usambazaji wa picha za ngono.
Faida za Google Glass
Wataalamu mbalimbali waliopata fursa ya kutumia
teknolojia hiyo, walisema itakuwa na faida nyingi hasa katika uwanja wa elimu.
Kwa mfano walisema mwalimu mmoja anaweza kutumika
kufundisha somo moja kwa wanafunzi waliopo sehemu mbalimbali duniani kwa
gharama kidogo.
Kwa kutumia teknolojia hiyo wanafunzi wanaweza
kusikia sauti na kuona kwa vitendo picha ama vielelezo anavyovitumia mwalimu
katika kurahisisha uelewa.
Mmoja wa wataalamu waliofanyia majaribio
teknolojia hiyo ni Dk Rafael Grossmann, ambaye aliandika kwenye mtandao wake wa
kijamii kuwa itasaidia kuwafundisha wanafunzi wake hata wakati anamfanyia
upasuaji mgonjwa bila wao kuwepo.
Jambo jingine la faida kwa teknolojia hii ni
katika tiba. Inaelezwa kuwa kwa kutumia kifaa hiki daktari moja bingwa anaweza
kuhudumia hospitali nyingi akiwa ofisini kwake.
No comments:
Post a Comment